To advertise here, call: +255 655 611699

Kilimo cha mbogamboga mkombozi wa ajira kwa vijana


 KILIMO kinatajwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kikichangia takribani nusu ya Pato zima la Taifa na robo tatu ya bidhaa zote zinazouzwa nje ya nchi. Pamoja na kuzalisha chakula, kilimo vilevile kinatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania. Sehemu kubwa ya kilimo Tanzania ni cha wakulima wadogo-wadogo (small-holder farmers) ambao wengi wao huwatumii njia za kisasa. Takwimu za Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania wakulima wake hulima hekta milioni 5.1 nchi nzima kila mwaka, na kati ya hizo asimilia 85 ni kwa ajili ya mazao ya chakula tu. Miongoni mwa mazao hayo ya chakula ni mazao yanayohusiana na mboga na matunda ambayo huzalishwa kwa wingi karibu katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani (Unguja na Pemba). Kilimo cha mboga na matunda kimekuwa maarufu nchini kutokana na sababu kadhaa, kama kuongezeka kwa mahitaji katika soko la ndani na nje,kuongezeka elimu kwa wakulima, upatikanaji kwa urahisi wa pembejeo na uwezeshaji wa unaofanywa na serikali na taasisi binafsi. Kutokana na sababu hizo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini (Arusha, Manyara, na Kilimanjaro) kilimo hiki kimeanza kuvuta kwa kasi makundi ya kijamii kama vijana na wanawake ambao sasa wamegeukia kilimo hicho hasa kufuatia uelimishaji na uhamasishaji unaofanywa na Chama cha Wakulima wa Maua, Mboga na Matunda Tanzania (TAHA). Chama hicho kimekuwa mstari mbele katika kuwapatia wakulima mazao ya mboga na matunda, elimu bora ya kilimo hicho, masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi, pembejeo na madawa muhimu na ushauri wa kitalaamu unaotolewa na maafisa ugani. Vijana wachangamkia fursa: Alfred Ole Laibanguti (40) ni mkazi wa kijiji cha Lakitatu wilayani Arumeru amekulia katika jamii ya wafugaji wa Kimaasai na katika makuzi yake hakuwahi kuwaza kama kuna shughuli nyingine anaweza kufanya zaidi ya ufugaji. Lakini kadri siku zilivyokuwa zinakwenda maisha yalimbadilisha Laibanguti na hivi sasa amekuwa mkulima wa mboga mboga wa kupigiwa mfano katika katika kijiji hicho kilichopo katika Kata ya Usa River, wilayani humo. Kwa kauli yake mwenyewe anakiri kuwa “kilimo cha mboga mboga kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji (drip irrigation) kimebadilisha maisha yangu kwa kiwango nisichoweza kuelezea”. Mkulima huyo alikuwa anazungumza na kundi la waandishi wa habari kutoka mkoani Arusha waliotembelea wakulima wa mboga na matunda katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara. Akitoa mfano, alisema kuwa analima nyanya kwenye eneo la ekari moja na robo ambayo amefunga mipira ya kumwagilia kwa njia ya kisasa na kuhudumia shamba lake kwa gharama ya shilingi milioni tatu na wakati wa mavuno anapata tani 20 ambazo kwa bei ya shambani anapata milioni 14. “Hii napata kwa musimu mmoja na mimi nalima kwa kipindi chote cha mwaka kwa sababu maji ya kumwagilia yapo muda wote,” Laibanguti alisema, akisisitiza kuwa ameweza kusomesha watoto, kujenga nyumba ya kisasa na kuwa na akiba ya kumsaidia wakati wa dharura. Kijana mwingine mwenye mafanikio ya kutolewa mfano ni Yusuf Yassin (29) mkazi wa kijiji cha Matufa Mkoani Manyara ambaye alibainisha kuwa kilimo hicho kimekuwa “muaarobaini” wa tatizo sugu la ajira nchini ambalo linawakabili vijana wengi. “Nilianza kilimo hiki miaka mitatu iliyopita, kwa kweli kiuchumi hali yangu imebadilika sana kutokana na mazao ninayozalisha kama nyanya, na aina nyingine tofauti za mboga kuuzika kwa haraka na kuwepo kwa soko la uhakika hasa kwa msaada wa TAHA,” alisema Yasin. “Vijana wengi wanalalamika kuwa hawana mitaji ya kuanzisha shughuli za kilimo, malalamiko yao hayana mantiki sana kwasababu vijana wengi wanamiliki simu za bei mbaya, nguo za thamani na kwa wakati moja unaweza kumkukuta kijana amevalia nguo na simu zote zikiwa na thamani ya kati ya shilingi laki tano hadi milioni moja, ”anaeleza zaidi. Kwa mujibu wa Yasin, kilimo cha mboga ni rahisi sana kwa sababu hakihitaji eneo kubwa la ardhi, na pia mazao ya aina hiyo hukomaa ndani ya siku kati ya 80-90 na mkulima anakuwa ameshapata fedha za mauzo na kurudisha gharama zake. “Katika eneo hili kuna vijiji zaidi ya 10, ambavyo wakulima wadogo wadogo wanalima mazao ya mboga mboga, na walioko chini yangu ni 96 ambao nawasimamia kwa kuwapa ushauri wa kitalaamu kuhusu kilimo hiki kuanzia hatua utayarishaji wa shamba, utambuzi wa mbegu bora, matumizi ya viatilifu na mambo mengine muhimu”alisema. Kijana mwingine Donald Munisi (36) mkazi wa kijiji cha Lakitatu wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha anabainisha kuwa kilimo cha mboga na matunda ni mkombozi wa kiuchumi kwa wakulima wengi. “Zamani changamoto kubwa ilikuwa ni masoko, lakini siku hizi kuna ongezeko kubwa sana la watu na pia mahoteli ya kitalii ambao wanaohitaji chakula, hivyo masoko si tatizo tena kama miaka ya nyuma,”anasema Munisi. Katika shamba lake la ekari tano, Munisi hulima aina mbalimbali za mboga na matunda, na amekuwa akipeleka sokoni mazao yake kila wiki kutokana na kuwa mipango mizuri na kuweka uwiano katika kupanda aina tofauti za mboga na kuvuna. Tatizo la Miundo Mbinu: Katika vijiji vyote ambavyo waandishi wa habari walitembelea changamoto kubwa inayowakabili wakulima ni tatizo la miundo mbinu ya barabara zisizopitika kabisa kwa gari hivyo wengi kushindwa kufikisha mazao yao katika masoko kwa muda. Katika kijiji cha Lakitatu na vijiji vya jirani barabara zake hazipitiki, kwa urahisi kutokana na kutofanyiwa matengenezo wala ukarabati kwa muda mrefu hivyo kuwa kikwazo kwa wakulima na hivyo kuwaongezea gharama zaidi kusafirisha mavuno yao kwenda sokoni. “Kama unavyoona hali ya barabara ni mbaya sana, hasa wakati wa masika barabara hazipitiki kabisa na hii ni changamoto kubwa sana kwa sisi wakulima, gharama zinaongezeka na matokeo yake faida pia inapungua”alisema moja wakulima wa nyanya. Aliongeza:”Halmashauri ya Wilaya imesahau maeneo ya wakulima ambayo yanazalisha mazao ya biashara na chakula, tumelalamikia hali hii kwa muda mrefu na hata viongozi wetu (Diwani na Mbunge) wanajua ila hakuna hatua zilizochukuliwa”. Taha wajizatiti: Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa TAHA, Sirila Mlay, anabainisha kuwa mipango ya taasisi hiyo ni kuwafikia wakulima wengi zaidi katika maeneo yote ambayo kilimo cha mboga na matunda kinaweza kufanyika. “Sasa tunaelekeza nguvu zetu katika maeneo yote ambayo kilimo kinaweza kufanyika, malengo yote ni kuwahusisha zaidi vijana na wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa tatizo la ajira nchini na tunadhani kwamba sekta hii inaweza kuwa mkombozi wa tatizo la ajira na kupunguza umaskini,”alisema. Mlay alieleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za za Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana kila mwaka idadi ya vijana wanahitimu elimu ya vyuo vikuu na vya kati inaweza kufikia milioni 1.2 na wanaofanikiwa kupata ajira katika sekta ya umma na binafsi hawazidi vijana 200,000. “Kwa takwimu hizo ni wazi kuwa kuna changamoto kubwa sana hivyo TAHA tunaamini kuwa tukishirikiana na serikali na wadau wengine basi tutatalipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo hili,” alisema. Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAHA, Anthony Chamanga, alieleza kuwa changamoto kubwa iliyokuwa ikiikabili sekta hiyo ni tozo mbalimbali za kodi za serikali katika sekta hiyo ambazo hata hivyo zimeondolewa katika bajeti ya kuu iliyotangazwa wiki iliyopita. “Tunaishukuru serikali yetu kwa namna ya kipekee tozo hizo zilikuwa kikwazo kikubwa sana kwa wakulima na wadau wa kilimo cha mboga,matunda na maua ambao ndiyo wanachama wetu, kwahiyo sasa tutarajie kukua kwa kasi zaidi kwa sekta hii”alisema. Kwa mujibu wa taarifa ya Gavana wa Benki ya Tanzania, Profesa Beno Ndulu, mwaka jana kuhusu hali ya uchumi wa nchi alisema mchango wa kilimo katika kupunguza umasikini umeshuka kutoka asilimia 30 mwaka 1998 hadi asilimia 21 mwaka 2014. Profesa Ndulu alisema sekta ya kilimo imeonekana kupigwa kikumbo na sekta za utalii, dhahabu, viwanda na usafirishaji wa mizigo nje ya nchi. Kwa mujibu wa takwimu hizo sekta ya utalii iliingizia Taifa dola za Marekani bilioni mbili (Sh trilioni 3.6), dhahabu dola bilioni 1.7 (Sh trilioni tatu), viwanda dola bilioni 1.3 (Sh trilioni 2.3) na kilimo kinachoingiza dola milioni 830 kwa mwaka.
Share on Google Plus

About Funguka Tanzania

0 comments:

Post a Comment